Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Didier Gomes amesema amekitazama kikosi cha Jwanang Galaxy na kujifunza mambo kadhaa, kabla ya kukabiliana nacho Jumapili (Oktoba 17).
Simba SC itaanzia ugenini dhidi ya Mabingwa hao wa Botswana, kisha itarejea nyumbani Jijini Dar es salaam tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Pili ambao umepangwa kuunguruma Oktoba 24, Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kocha Gomes amesema Jwaneng Galaxy wana kikosi kizuri na anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwao, lakini akasisitiza kuwa, amejiandaa kukabiliana nao na kupata matokeo mazuri ugenini.
Amesema kikosi cha Jwaneng Galaxy kinacheza pasi fupi na kinashambulia kwa kasi, jambo ambalo amelifanyia kazi katika mazoezi ya kikosi chake kabla ya kuanza safari ya kuelekea mjini Gaborone leo Ijumaa (Oktoba 15).
“Nimeitazama Galaxy kupitia video ni timu nzuri, inashambulia kwa kasi pia wanazuia kwa pamoja kwa hiyo tunapaswa kuwa makini kuwadhibiti hatutakiwi kufanya makosa mengi ya ulinzi.”
“Malengo yetu ni kufika hatua ya makundi kwa hiyo inabidi tuchukue tahadhari zote bila kuangalia ukubwa wetu hatutaidharau Galaxy.” amesema Gomes.
Kikosi cha Simba SC tayari kimeshaanza safari ya kuelekea Gaborone, Botswana kikiwa na wachezaji 24 na maafisa wa Benchi la Ufundi linaloongozwa na Kocha Gomes.
Wachezaji waliosafiri upande wa Walinda Lango ni: Aishi Manula, Beno Kakolanya, Jeremiah Kisubi na Ally Salum.
Mabeki: Shomary Kapombe, Israel Mwenda, Mohamed Hussein, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Kennedy Juma, Inonga Varane na Joash Onyango.
Viungo: Thadeo Lwanga, Jonas Mkude, Sadio Kanoute, Rally Bwalya, Mzamiru Yassin, Ibrahim Ajibu, Hassan Dilunga, Bernard Morrison, Peter Banda, Duncan Nyoni na Abdul Swamadu.
Washambuliaji: Meddie Kagere, John Boko na Kibu Denis.