Mshambuliaji  kutoka nchini Burundi na klabu ya Azam FC, Didier Kavumbagu anaendelea kufanya mazungumzo na uongozi wa Mbeya City na amewataka wampe dola 40 elfu zaidi ya Sh 80 milioni ili amwage wino kwa ajili ya msimu ujao.

Fedha hizo zinaonekana kuwa nyingi mno kwa klabu changa kama Mbeya City ambapo sasa bado hawajaamua kama watamchukuwa ama wataachana naye kutokana na dau hilo kubwa.

Habari zilizopatikana ni kwamba, City wameamua kumwacha ili aamue kama atakubaliana na mapendekezo yao waliyompeleka kwenye mazungumzo yao ya awali ndipo watampa mkataba ikishindikana basi wataangalia ustaarabu mwingine.

Kavumbagu amemaliza mkataba na Azam hivyo ni mchezaji huru na inadaiwa kuwa matajiri hao hawana mpango wa kuendelea naye msimu ujao.

”Kavumbagu bado hajamalizana na Mbeya City kwani pesa aliyohitaji ya usajili ni kubwa mno na City hawana uwezo huo, hivyo wanaendelea na mazungumzo kama watafikia makubaliano basi atasaini mkataba wakishindwana basi kila mtu ataangalia ustaarabu wake,” kilisema chanzo hicho.

Azam walimsajili Kavumbagu akitokea Yanga ambao walishindwa kumwongeza mkataba kwa muda na hivyo kutimkia Chamazi.

Jose Mourinho Apanga Kumuhamishia Marco Verratti Old Trafford
Madereva wa Mabasi ya Mwendokasi wafanya ‘mgomo baridi’