Mshambuliaji raia wa Uhispania ambaye ametemwa kwenye kikosi cha Chelsea, Diego Costa amefungua mashtaka dhidi ya klabu hiyo kwa madai ya kuchelewa kumruhusu kuondoka.
Wiki iliyopita, mwanasheria wa Diego Costa, Ricardo Cardoso alikaririwa akitishia kuishtaki Chelsea kwa kushindwa kujibu taarifa rasmi ya maombi ya uhamisho wa Diego Costa kutoka kwa timu yake ya zamani ya Atletico Madrid.
Mwanasheria huyo amesema kuchelewa kwa majibu hayo kunatafsiriwa kama makusudi ya Kocha wa Chelsea, Antonio Conte kutaka kucheleshwa uhamisho wa mchezaji huyo.
Kwa mujibu wa Sportsmail, mashtaka dhidi ya Chelsea tayari yamekwisha wasilishwa ingawa kwa upande mwingine Antonio Conte akizungumza na waandishi wa habari alisema hafahamu lolote kuhusu kinachoendelea kuhusu taarifa hiyo.
Diego Costa ambaye ameichezea Chelsea michezo 89 na kufunga magoli 52 tangu alipo jiunga na matajiri hao wa jijini London mwaka 2014, amekuwa akimlaumu kocha Antonio Conte kwa kumpa taarifa za kumtema kupitia ujumbe mfupi wa simu.