Hali ya hofu imeendelea kutanda kwa meneja wa klabu bingwa nchini Uingereza, Chelsea, Jose Mourinho kufuatia kizungumkuti kinachomuandama mshambuliaji kutoka nchini Hispania, Diego Costa.

Mourinho, ameonyesha kuwa na hofu na mshambuliaji huyo kama ataweza kuwa sehemu ya kikosi chake mwishoni mwa juma hili wakati wa mchezo wa kwanza wa ligi ya Uingereza msimu huu, baada ya kushindwa kumtumia kwenye pambano la kuwania ngao ya jamii hapo jana dhidi ya Arsenal.

Mwishoni mwa juma lililopita, Jose Mourinho aliwathibitishia waandishi wa habari utayari wa mshambuliaji huyo kurejea tena uwanjani kufuatia hali yake ya majeraha ya nyama za paja, lakini jana alionekana akiwa benchi.

Hata hivyo, meneja huyo kutoka nchini Ureno amesema, ilikuwa ni vigumu kwake kumtumia Costa katika mchezo dhidi ya Arsenal kutokana na hali yake kiafya kubadilika dakika kadhaa kabla ya kwenda uwanjani.

Mourinho amesema hana haraka ya kumtumia Costa, zaidi ya kuheshimu ushauri ambao anaupokea kutoka kwenye jopo la madaktari klabuni hapo.

Kwa mantiki hiyo sasa, Costa anatarajiwa kuwa nje ya kikosi cha Chelsea ambacho kitapambana na Swansea City, kwenye mchezo wa ufunguzi wa ligi ya England mwishoni mwa juma hili.

Zitto Kabwe: Lowassa Na Magufuli Hawauwezi Ufisadi
Di Maria Atua Mjini Doha, Qatar