Mchezaji nyota wa zamani wa kandanda na moja ya wachezaji bora zaidi wa kandanda kuwahi kutokea, Diego Maradona amefariki dunia leo Novemba 25, 2020 akiwa na umri wa miaka 60.

Kiungo huyo mshambuliaji wa Argentina awali mwezi huu alifanyiwa upasuaji wa ubongo, ambao madaktari walimwambia ulifaulu na ilitangazwa kuwa baada ya upasuaji huo, angeanza matibabu ya uraibu wa pombe.

Mwaka 1986 akiwa nahodha wa Argentina, aliliongoza Taifa lake kushinda Kombe la Dunia nchini Mexico huku akionesha uwezo binafsi mkubwa katika ushindi huo.

Alizichezea klabu za Barcelona ya Uhispania na Napoli ya Italia ambapo akiwa na Napoli alinyakua ubingwa wa ligi ya Serie A kwa misimu miwili.

Maradona aliifungia Argentina magoli 34 katika michezo 91, akishiriki michuano minne ya Kombe la Dunia.

Alichaguliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Argentina mwaka 2008 na akaachana na kibarua hicho baada ya Kombe la Dunia mwaka 2010 ambapo Argentina ilitolewa na Ujerumani katika hatua ya robo fainali na baada ya hapo, alienda kuvinoa vilabu kadhaa katika nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu na kisha Mexico.

Kwa wengi, Maradona anatajwa kuwa ndiye mchezaji wa mpira wa miguu bora zaidi kuwahi kutokea (The Best Ever), na kwa umahiri wake alipewa jina la  “El Pibe de Oro” (The Golden Boy).

Maradona, ambaye ni mmoja kati ya wachezaji wawili walioshinda tuzo ya FIFA ya Mchezaji Bora wa Karne ya 20, alizaliwa Oktoba 30 mwaka 1960 na mpaka umauti unamfika alikuwa na timu ya Gimnasia y Esgrima inayoshiriki ligi kuu ya Argentina.

Pumzika kwa Amani, Diego Armando Maradona Franco ??

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 26, 2020
WHO : Ulaya yapata ahueni