Ni kama dili la usajili wa Mshambuliaji wa Klabu ya Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland, kwenda Chelsea limeyeyuka, kufuatia sababu kadhaa zinazotajwa.
Chelsea wanahusishwa na mpango wa kumsajili Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20, katika kipindi hiki cha dirisha kubwa la usajili kuelekea Msimu wa 2021-22.
Sababu mojawapo inayotajwa kufanya dili hilo kuwa gumu ni kuondoka kwa Jadon Sancho aliyejiunga na Man United, hivyo Uongozi wa Dortmund umeona itakua vigumu kwao kuingia katika mazungumzo ya kumuuza Haaland.
Wanaamini endapo watafanya hivyo, kikosi chao kitakosa makali kwenye eneo la ushambuliaji msimu ujao ambalo litakua limepoteza watu wawili muhimu.
Mbali na sababu hiyo, sababu nyingine inayotajwa kuwa kikwazo katika uhamisho wa Haaland ni klabu ya Chelsea inaweza ikakumbana na adhabu ya matumizi ya pesa nje ya utaratibu kutoka UEFA.
Klabu hiyo ya jijini London msimu uliopita tu, ilitumia kiasi kikubwa cha pesa kusajili mastaa kadhaa wakiwamo Kai Havertz na Timo Werner, hivyo wakijitumbukiza kwa Halaand watajitia kitanzi kisheria.