Kampuni ya Vanguard imetangaza ‘dili’ kwa wafanyakazi wake ambao watapata chanjo ya corona, kila mmoja atalipwa $1,000 (sawa na Sh. 2,319,000 za Tanzania).
Kampuni hiyo ambayo ni moja kati ya makampuni yenye uwekezaji mkubwa zaidi duniani, ina wafanyakazi zaidi 16,500 nchini Marekani. Imesema inaamini kupata chanjo ya corona ni njia sahihi zaidi ya kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona. Hivyo, inawahamasisha wafanyakazi wake kupata chanjo hiyo.
“Vanguard tunatambua kuwa chanjo ya corona ni njia sahihi zaidi ya kupambana na kusambaa kwa virusi na tunawapa hamasa zaidi wafanyakazi wetu kupata chanjo. Kwahiyo, tunatoa stahiki kwa wafanyakazi ambao watawasilisha ushahidi wa kupata chanjo,” msemaji wa Vanguard, Charles Kurtz anakaririwa.
Kwa mujibu wa Bloomberg News, Vanguard imeeleza kuwa imetenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya kuwapongeza wafanyakazi ambao wanathamini kujilinda na kuilinda jamii inayowazunguka.
Kampuni hiyo ni moja kati ya makampuni makubwa ambayo yameweka masharti kwa wafanyakazi wake kuhakikisha wanapata chanjo ya corona. Makampuni mengine makubwa ni Microsoft na Google ambao wameweka sharti la lazima kwa kila mfanyakazi kupata chanjo.
Walmart na Uber wao wamewataka wafanyakazi walio kwenye ngazi ya Menejimenti, sio wafanyakazi wa kawaida, kuhakikisha wanapata chanjo ya corona, wakati Amazon na Apple wao hawana sera ya corona hadi sasa.
Tanzania pia imefuata nyayo za dunia ambapo Serikali imesema kuchanja ni hiari na hakuna atakayelazimishwa.
Hata hivyo, hali imeanza kuonekana kuwa huenda siku za usoni kukawa na masharti madogo-madogo yatakayowanyima fursa watu ambao hawajachajwa. Hivi karibuni, Wizara ya Maliasili na Utalii ilieleza kuwa kundi kubwa la wageni waliongia nchini kwa ajili ya utalii watahudumiwa na wafanyakazi ambao wamepata chanjo ya corona.
Watanzania wengi wamejiandikisha na wengi wamejitokeza kupata chanjo katika mikoa mbalimbali nchini, tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan achanje na kuwahamasisha watanzania wengine kuchukua hatu hiyo.