Kiungo Mshambuliaji wa Simba SC Hassan Dilunga ataendelea kuwa nje ya kikosi cha klabu hiyo, kwenye mchezo wa ‘Kundi D’, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa Mzunguuko wa 04 wa Kundi D, Kombe la Shirikisho utakaopigwa Jumapili (Machi 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam, huku ikiwa na deni la kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0, kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 03 wa Kundi D, uliounguruma mjini Berkane-Morocco Februari 27.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amezungumza na WASAFI MEDIA mapema leo Jumatano (Macho 09), na kuthibitisha taarifa za kiungo huyo kukosekana kwenye mchezo huo kufuatia kuwa na majeraha ya mguu.
Amesema Dilunga kwa sasa anaendelea na matibabu, hivyo ni mapema mno kusema lini atajiunga na wenzake, licha ya kufahamika hatokuwa sehemu ya kikosi siku ya Jumapili (Machi 13) Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mbali na Dilunga, Ahmed amesema Simba SC itaendelea kukosa huduma ya kiungo kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama, kufuatia kanuni za usajili wa Michuano ya Kombe la Shirikisho kumuengua.
Katika hatua nyingine Ahmed amesema sehemu kubwa ya wachezaji waliokua majeruhi wamerejea kikosini na wanaendelea na maandalizi ya kuikabili RS Berkane Jumapili (Machi 13).
“Waliorejea kikosini ni Mshambuliaji Kibu Denis ambaye alikosekana kwa kipindi kirefu baada ya kuumia mwezi Januari wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City, Chriss Mugalu naye yuko sawasawa kabisa, baada ya kuumia kidole akiwa kwenye majukumu ya kuikabili Mbeya City.”
“Wasiwasi watu walionao kwa sasa ni kwa John Bocco baada ya kutolewa nje kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji FC, lakini niwaeleze tu, nahodha wetu tutakuwa naye, Shomari Kapombe ambaye aligongana na Atupele Green kwenye mchezo dhidi ya Biashara United Mara naye upo vizuri, Jonas Mkude naye yupo vizuri baada ya kupata homa kali tulipokuwa safarini Niger na Morocco.”
“Niseme tu, RS Berkane wamekuja wakati mbaya, kwa sababu asilimia kubwa ya wachezaji wa Simba SC wako FIT, tena wakiwa na kiu ya kulipa kisasasi cha kufungwa mabo mawili na hawa hawa jamaa.” amesema Ahmed
Simba SC itakua na kazi kubwa ya kusaka ushindi kwenye mchezo dhidi ya RS Berkane ili kujitengenezea njia nzuri ya kufuzu hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho, huku wageni wao kutoka Morocco wakiwa na lengo kama hilo.
Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, unaonyesha kuwa RS Berkane inaongoza ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama o4 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia ikiwa na alama 03.