Kiungo Mshambuliaji wa JKT Tanzania, Hassan Dilunga, atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu akiuguza jeraha la enka ya mguu wa kulia.

Dilunga aliumia enka katika mchezo wa JKT Tanzania dhidi ya Dodoma Jiji FC uliochezwa Oktoba 30, mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, ambapo JKT ilikubali kichapo cha 1-0.

Akizungumza jijini Dar es Salaam Ofisa Habari wa JKT Tanzania, Masau Bwire, amesema Dilunga alipata jeraha hilo lililosababisha kuvunjika kwa mfupa mdogo ambao husaidia mfupa mkuu kufanya kazi.

“Kwa sasa amefungwa bandeji ndogo atakayokaa nayo kwa juma moja, baada ya hapo atafungwa kubwa itakayoondolewa baada ya mwezi mmoja na ataanza mazoezi mepesi baada ya miezi miwili.

“Atakaa sawa na kurudi uwanjani kucheza mpira baada ya miezi mitatu tunamwombea aweze kupona haraka na arejee katika majukumu yake ya kawaida,” amesema

Dilunga ambaye pia ana uwezo wa kucheza kama Mshambuliaji namba mbili amejiunga na JKT Tanzania Julai mwaka huu akitokea katika kikosi cha Simba SC.

Kichapo chamchefua Mikel Arteta
Watatu jela miaka 30 kwa unyang'anyi, ubakaji