Kiungo mshambuliaji wa mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC Hassan Dilunga amefurahishwa na kitendo cha kiungo zamani wa klabu ya Everton ya England Timothy Filiga Cahill kuretweet video iliyokua akishangilia bao alilowafunga Mtibwa Sugar kwenye mchezo wa ligi kuu msimu huu.
Dilunga alifunga bao la tatu dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa mzunguuko wa pili uliochezwa Uwanja wa Jamuhuri mjini Morogoro mapema mwaka huu, ambapo Simba walichomoza na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri, huku mabao mengine yakifungwa na nahodha John Bocco na Mohamed Hussein.
Cahill ameretweet video hiyo kupitia ukurasa wa @SimbaSCTanzania, hatua ambayo imedhihirisha amependezwa na kitendo cha Dilunga kushangilia kama alivyokua akifanya yeye alipokuwa dimbani na kuzifumania nyavu za timu pinzani.
Katika video hiyo @SimbaSCTanzania waliandika “Siku ligi ikirudi, kazi ni moja tu, mpaka tushinde ubingwa #NguvuMoja.”
Akizungumzia hatua ya Cahill kuretweet video hiyo Dilunga amesema: “Nashukuru mwenyezi mungu kwa kipindi hiki, kwa sababu ni kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, pili nilivyoona mwili wangu ulisisimka kwa sababu sikuamini kama Cahill angeweza kuretweet.”
“Nilipokua nashangilia niliona ni jambo la kawaida lakini kwa hatua ya mchezaji kama Cahil kuretweet imenionyesha nilifanya jambo kubwa ambalo limemgusa gwiji mkubwa wa soka duniani.”
Hata hivyo Dilunga amesema baada ya kushangilia bao kwa aina alivyofanya, baadhi rafiki zake walimtaka kuendelea kufanya hivyo, kwa sababu walipendezwa na walimtajia wachezaji waliowahi kufanya kitendo kama hicho akiwepo Tim Cahill.
“Rafiki zangu walishauri aina hiyo ya ushangiliaji ninapaswa kuiendeleza kwa sababu iliwafurahisha, pia waliniambia baadhi ya wachezaji wakubwa duniani ambao wamewahi kuitumia, na mimi niliwahakikishia kuendelea kufanya hivyo nitakapopata nafasi ya kucheza na kufunga mabao, endapo sitokua na kitu kingine za kufikisha ujumbe kupitia mazingira yanayonizunguuka, nitashangilia kama walivyonishauri.”
Mbali na klabu ya Everton ambayo aliitumikia kuanzia mwaka 2004–2012 (Michezo 226, Mabao 56), Tim Cahill amewahi kuzitumikia klabu nyingine kama Millwall 1998–2004 (Michezo 217, Mabao 52), New York Red Bulls 2012–2015 (Michezo 62, Mabao 14), Shanghai Shenhua 2015–2016 (Michezo 28, Mabao 11), Hangzhou Greentown mwaka 2016 (Michezo 17, Mabao 4) na Melbourne City 2016–2017 (Michezo 28, Mabao 11)
Mwaka 2018 alirudi Millwall 2018 na kucheza michezo 10 na baadae alihamia Jamshedpur 2018–2019 (Michezo 11, Mabao 2).
Upande wa timu ya taifa ya Australia Tim Cahill alicheza kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 23 kuanzia mwaka 2004. Alicheza michezo mitatu na kufunga bao moja.
Baadae alianza kuitumikia timu ya taifa ya wakubwa ya taifa hilo kuanzia mwaka 2004–2018, ambapo alifunga mabao 50 katika michezo 108.