Uamuzi wa meneja wa Man City Pep Guardiola kutomjumuisha kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast Yaya Toure katika kikosi cha klabu hiyo kitakachoshiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kimezua hisia tofauti kwa mashabiki wa soka barani Afrika.

Baadhi ya mashabiki wa soka kutoka barani humo, wanaamini maamuzi ya Guardiola yanachangiwa na chuki zake binafsi kwa wachezaji wa Afrika jambo ambalo linaahisiwa huenda likaipunguzia Man City mashabiki kutoka ukanda huo.

Wakati hisia hizo zikichukua nafasi miongoni mwa mashabiki wa soka kutoka barani Afrika, wakala wa Toure, Dimitri Seluk anaamini Toure amedhalilishwa kwa kutoswa bila kuambiwa.

Seluk ameungana na mashabiki wanaoamini kubaguliwa kwa Toure, kitaipunguza Man City wapenzi kutoka Afrika, hususana katika kipindi hiki cha kuelekea mchezo wa ligi kuu ya England dhidi ya ManUtd ambao utachezwa mwishoni mwa juma hili.

“Manchester City itapoteza mamilioni ya mashabiki wa Afrika kwa sababu ya uamuzi wa Guardiola,” wakala wa Toure ameuambia mtandao wa Sportsmail.

“Wataanza kuishabikia Manchester United. Watu wengi Afrika wanasema hawataangalia tena michezo ya Manchester City kwenye televisheni.”

Hii si mara ya kwanza kwa Pep Guardiola kumuengua Toure katika mipango yake, kwani aliwahi kufanya hivyo akiwa FC Barcelona na kufikia hatua ya kuchagiza mpango wa kuuzwa kwake na kuelekea Man City mwaka 2010.

Simba SC Yatoa Shukurani Kwa Mashabiki Wa Dodoma
Salum Mwalimu, Wafuasi Chadema wapata dhamana, ni baada ya Ukuta kuwaweka selo