Dirisha la uombaji mikopo ya Elimu ya juu, kwa mwaka 2022/2023 linatarajia kufunguliwa kabla ya Julai 15, 2022.

Taarifa ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), iliyotolewa Julai 6, 2022 na Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru imesema HESLB inakamilisha taratibu za uombaji mikopo kwa mwaka 2022/2023 na dirisha litafunguliwa katika kipindi cha siku 10 zijazo.

“Taarifa hii inatolewa kufuatia maombi mengi ya taarifa ya ufafanuzi kutoka kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka 2022 na matokeo yao kutangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA),” amesema Mkurugenzi Badru.

Baadhi ya Wanafunzi wa Elimu ya juu, wakiwa nje ya jengo la Bodi ya mikopo ya elimu ya juu HESLB.

Badru ameongeza kuwa, kwa sasa waombaji mikopo wanatakiwa kuanza maandalizi ya awali ya kuandaa nyaraka muhimu kama vyeti vyao vya kuzaliwa au vyeti vya vifo vya wazazi wao vilivyohakikiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), na Wakala wa Usajili wa Matukio Muhimu Zanzibar (ZCSRA).

Akizungumzia suala la sifa na utaratibu wa kuomba mkopo kwa mwaka 2022/2023, Badru amesema maelezo yatapatikana katika mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka 2022/2023, utakaoanza kupatikana katika tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz Julai 15, 2022.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ilianzishwa mwaka 2005 kwa minajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wanaojiunga na taasisi za elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanufaika.

Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru

Tanzania, Afrika Kusini zasaini makubaliano ya Elimu Kiswahili
Chriss Mugalu azigonganisha Zambia, DR Congo