Mshambuliaji wa zamani wa Majogoo wa Jiji ‘Liverpool’ Dirk Kuyt, anaamini Meneja Erik Ten Hag kutoka Uholanzi, atakua chaguo sahihi kwa Manchester United, ambayo inatajwa kuwa mbioni kumuajiri mwishoni mwa msimu huu.
Ten Hag anatajwa kuwindwa huko Old Trafford, kufuatia ufanisi wake wa kazi akiwa Ajax Amsterdam, huku asilimia kubwa ya viongozi wakiafiki jina lake kupitishwa ili kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi klabuni hapo.
Kuyt amezungumza na Waandishi wa Habari na kusema: “Ten Hag ni meneja bora, mwenye uzoefu, tayari amejifunza vya kutosha, amefanya kazi kwenye klabu ya Bayern Munich kama kocha msaidizi, baadaye Utrech na sasa Ajax.
“Ni meneja bora ambaye amejiimarisha sana, ndani na nje ya uwanja. Najua kuna watu wana wasiwasi na uzungumzaji wake wa lugha ya Kingereza, jinsi anavyozungumza mbele ya kamera, lakini unaona jinsi anavyoimarika siku hadi siku kama kocha na nadhani anaweza kuwa kocha bora kwenye timu yoyote kubwa Ulaya.
“Mbinu zake, jinsi anavyofikiria kuhusu mpira, inavutia, na itakuwa vizuri kama atapata nafasi ya kufundisha timu kubwa.”
Licha ya Ten Hag kupewa kipaumbele cha kuwa Meneja wa kikosi cha Man Utd msimu ujao, pia ana upinzani kutoka kwa mameneja wengine ambao wanatajwa kuiwania nafasi hiyo ambao ni Mauricio Pochettino, Luis Enrique na Julen Lopetegui.