Nahodha na mshambuliaji kikosi cha Feyenoord Dirk Kuyt ameshangazwa na kauli iliyotolewa na mchezaji ghali duniani kwa sasa Paul Pogba, mara baada ya mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa hatua ya makundi ya michuano ya Europa league uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo mjini Rotterdam nchini Uholanzi.

Katika mchezo huo Man Utd walikubali kibano cha bao moja kwa sifuri lililofungwa na Tonny Vilhena.

Kuyt amesema mara baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa alizungumza na Pogba na hakuamini alichoambiwa na kiungo huyo kuhusu uwezo na umakini aliouonyesha katika mchezo huo, ambao ulishuhudia meneja wa Man Utd akifanya mabadiliko ya wachezaji wanane katika kikosi cha kwanza, tofauti na ilivyokua mwishoni mwa juma lililopita wakati wa mchezo wa ligi ya England dhidi ya Man City.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 36, amesema Pogba alimsifia kwa kusema hakuamini kama angeweza kumuona Kuyt akiwa katika kiwango kizuri na kuwa msaada mkubwa kwa Feyenoord kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

“Aliniambia ‘Inashangaza’, hakuamini kama bado nina uwezo mkubwa wa kucheza soka kwa kuzunguuka uwanja wote tena kwa kasi ya ajabu, jambo ambalo ni tofauti na umri wangu” alisema Kuyt

“Aliendelea kubainisha kuwa, inapendeza kuniona nikiwa katika hali kama ile, na kwa upande wangu nimefarijika kusikia maneno hayo yakitoka kwa mchezaji ambaye kwa sasa ndio gumzo duniani.” Aliongeza Kuyt

Kuyt aliwahi kucheza soka nchini England akiwa na klabu ya Liverpool kuanzia mwaka 2006 hadi 2012 na alifanikiwa kucheza michezo 286 huku akifunga mabao 71.

Baada ya kuondoka Anfield, Kuyt alielekea nchini Uturuki kujiunga na klabu ya Fenerbahçe na mwaka 2015 alirejea nyumbani kwao Uholanzi baada ya kusajiliwa na Feyenoord.

Radio 5 yafungiwa miezi 3, yapigwa faini ya sh. mil.5
Mbowe roho juu, hukumu yake kusomwa leo.