Diwani wa Kata ya Mkambarani (CCM), iliyopo Wilaya ya Morogoro, Charles Mboma ameandika barua ya ajiuzulu akidai kuwa Viongozi wa juu kushindwa kutatua changamoto za Kata hiyo, pindi anapoziwasilisha ikiwemo migogoro ya ardhi na mabadiliko ya Uongozi yasiyoleta tija kwa Wananchi.
Mboma ameyasema hayo wakati akizungumza na Wanahabari na kudai kuwa maamuzi hayo amechukua bila kushauriwa na mtu na kwamba barua hiyo ameilekeza kwenye uongozi wa Chama Kilichompa dhamana, ngazi ya Kata na Wilaya, ili kuwatarifu.
Amesema, mara kwa mara amekua akitoa taarifa za changamoto za kata yake ikiwemo migogoro ya ardhi na kuziwasilisha kwa uongozi wa Serikali Ngazi ya Wilaya na kushindwa kutatuliwa, huku Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi Kata ya Mkambarani, Bill Numbi akithibitisha kupokea barua hiyo.
Charles Mboma, alichaguliwa 2020 na amehudumu kwa kipindi cha miaka mitatu na amesisitiza Mamlaka zinazofanya teuzi kutobadili viongozi mara kwa mara kwani yeye kwa kipindi hicho cha uongozi amefanya kazi na Wakuu wa Mikoa wanne na Wakuu wa Wilaya Wanne na kila kiongozi huja na vipaumbele vyake bila kutatua changamoto za Wananchi.