Aliyekuwa Mtangazaji na mchezea santuri wa Clouds Fm Radio, DJ Fetty amejitenga na lawama zinazotolewa na mashabiki kwenye mitandao ya kijamii wakimtaka kumsaidia rapa Godzilla kutokana na mitazamo yao kuwa hayuko sawa.
Lawama hizo kwa Fetty zilianza kutiririshwa na mashabiki punde baada ya Godzilla aka King wa Salasala kufanya mahojiano na kipindi cha XXL, ambapo wengi hawakuridhishwa na jinsi walivyomsikia kwa kulinganisha na Godzilla waliyekuwa wanamfahamu awali.
Kwa mujibu wa Fetty, lawama zilizokuwa zikielekezwa kwake za ‘kwanini hamsaidii Zilla’, zilirejea historia ya kuwa yeye ndiye aliyefanikisha kumuweka kwenye ramani ya muziki kupitia mashindano ya kufanya mitindo huru (Freestyle Battle).
Akifunguka leo kupitia kipindi cha Bongo Fleva ya redio hiyo, Fetty amesema kuwa yeye hana uwezo wa kumbadili msanii huyo au kumwambia kuwa ana tatizo kwani suluhu inapaswa kuanza na utambuzi wake wa tatizo.
“Mimi sina uwezo wa kucontrol maisha yake. Sina uwezo wa kufuatilia maisha yake. Na mimi naona sina uwezo wa kukaa chini na Zilla na kumfanya anielewe mimi,” alisema Fetty.
“Kama kweli anahitaji mtu wa kumsaidia. Unajua ni lazima mtu ajue kama ana tatizo ndio atasaidiwa. Sasa kama mtu hajajua mwenyewe hawezi kumsikiliza mtu mwingine. Hata wewe ukinifuata mimi ukaniambia kwamba mimi ni chizi na mimi sijaona hivyo, ninaweza kukumind,” aliongeza.
Hata hivyo, Fetty alieleza kuwa aliona mabadiliko kwa msanii huyo lakini alidhani labda U-Marekani unamkorea tu, kwa kuongeza ‘swag’ za kimarekani kwenye mazungumzo yake na kadhalika.
Alishauri pia kuwa kama watu wanaamini Zilla ana tatizo, wanaoweza kumsaidia zaidi ni watu wazima anaowakubali na kuwaheshimu. Hivyo, kama kuna namna njia hizo zifuatwe badala ya kumshushia lawama yeye kwakuwa tu alimpa njia ya kupitia ambayo awali aliitumia vizuri na kushinda shindano la Freestyle Battle na kisha kuachia ngoma nyingi kubwa.
Uwezo wa Godzilla katika kufanya mitindo huru ni wa kipekee na wakati mwingine huwafanya watu kuhisi alikuwa ameandika mistari kabla, lakini katika kipindi cha hivi karibuni ameonekana kushindwa kuonesha uwezo aliokuwa nao hasa aliposikika kwenye mahojiano na vyombo kadhaa vya habari.