Tetesi za soka zinaeleza kuwa mshambuliaji kutoka nchini Ivory Coast Richard Djodi ameachana na Azam FC, kufuatia mkataba wake kuvunjwa na uongozi wa klabu hiyo, ili kutoa nafasi ya usajili wa mchezaji mwingine wa kigeni ndani ya kikosi cha klabu hiyo.
Mshambuliaji huyo aliyejiunga na Azam FC mwaka 2018 akitokea Ashanti Gold ya Ghana amefikia makubaliano ya kuvunjwa kwa mkataba wake, na tayari ameshaondoka nchini tangu juma lililopita.
Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa, Azam FC wamepanga kujaza nafasi ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, kwa kufanya usajili wa mlinda mlango kutoka nje ya mipaka ya Tanzania.
Azam FC tayari ilikuwa na wachezaji kumi wa kigeni ambao ni Daniel Amoah, Obrey Chirwa, Prince Dube, Ally Niyonzima, Nicholas Wadada, Bruce Kangwa, Never Tigere, Yakubu Mohammed, Mpiana Moziz na Djodi (ambaye ametemwa), hivyo kwa mujibu wa kanuni za Bodi ya Ligi nchini (TPLB), inaitaka kila klabu kusajili wachezaji wakigeni 10 pekee, jambo ambalo klabu hiyo ilipaswa kupunguza waliopo ili kupata nafasi mpya ya kusajili.
Afisa Mtendaji wa Azam FC Popat amesema baada ya Kocha Mkuu, George Lwandamini, kuona upungufu uliopo katika kikosi chake, alihitaji kusajiliwa mshambuliaji, hivyo kumsajili Mpiana huku suala la kipa likiwa katika mchakato.
“Kulingana na idadi ya wachezaji 10 wa kigeni walikuwapo ndani ya timu, lazima mmoja atoke ili mwingine aingie, kwa sasa ni mapema kutaja ni nani ila mambo yakiwa sawa tutaweka wazi ni mchezaji gani,” amesema Popat.
Uongozi wa Azam FC umejipanga kukitumia kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili kuboresha kikosi chao kinayochonolewa na kocha Lwandamina, ili kurejesha makali ya kuwa sehemu ya timu zinazowania ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu 2020/21.
Azam FC ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikwa na alama 28, ikitanguliwa na mabingwa watetezi Simba SC wenye alama 32, huku Young Africans wakiongoza msimamo wa Ligi hiyo kwa kumiliki alama 43.