Beki wa pembeni kutoka DR Congo Djuma Shaaban amefunguka kwa mara ya kwanza mazingira yaliyomfanya kuondoka kwa mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans mwanzoni mwa msimu huu 2023/24.

Beki huyo anayecheza upande wa kulia, aliondoka klabuni hapo sambamba na Kiungo Yannick Bangala ambaye alitimkia Azam FC, iliyomsajili siku chache kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Djuma amesema kulikuwa na mazingira tatanishi kabla ya kuondoka Young Africans, huku akiweka wazi baadhi ya matukio ambayo yalidhihirisha ukomo wa maisha yake ndani ya klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Djuma Shaaban amesema: “Tuliporudi Tanzania kuendelea na mkataba wa mwaka ule ambao tuliongeza kuna mambo yaliibuka. Kulikuwepo tofauti kati ya meneja wetu mimi na Bangala (Yannick) alipotofautiana na uongozi wa Young Africans. Yale mambo yalikuwa mazito ikashindikana kupatikana muafaka kwa haraka.”

 “Mambo yaliyokuwa yanasemwa sitaki kuyaweka wazi ila yalinivunja nguvu na nikaona bora tufikie hatua ya kuachana. Tukakubaliana na uongozi kusitisha mikataba na tukaondoka,” amesema Djuma

Katika hatua nyingine Djuma Shaaban amefunguka sababu za kukosa sehemu ya usajili wa dirisha lililopita, kwa kusema alifanyiwa makusudi na Uongozi wa Young Africans ambao uliamini angejiunga na Simba SC, hali ambayo iliwafanya kuchelewesha barua ya kuthibitisha kuachana naye.

“Baada ya kuachana ugumu ukawa kunipa barua ya kuniacha. Nilikuwa tayari na ofa mbalimbali lakini Young Africans hawakutaka kunipa barua yangu. Niliambiwa na watu wangu kwamba walidhani ningekwenda Simba. Hatua ile ilinikosesha kupata timu haraka, nilipopewa barua muda wa usajili ulikuwa umekwisha ndio maana sina timu hadi sasa.” amesema Djuma

Kwa sasa Djuma Shaaban anahusishwa na mpango wa kusajiliwa Azam FC wakati wa Dirisha Dogo, na amekuwa akifanya mazoezi ya kikosi cha klabu hiyo na jana Jumapili (Novemba 19) alicheza mchezo wa Kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar ambayo ilikubali kufungwa 3-1.

Vinicius Jr kurudi dimbani Februari 2024
Waziri Mkuu wa zamani aweka mambo hadharani