Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi, anatarajia kumtumia Beki wa Kulia kutoka DR Congo Djuma Shaban kwenye mchezo wa mzunguuko wa 15 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.
Young Africans itakua mgeni wa Mtibwa Sugar siku ya Jumatano (Februari 23), katika Uwanja wa Manungu Complex mkoani Morogoro.
Djuma Shaban anatajwa kuwa kwenye mipango ya Kocha Nabi, kufuatia adhabu yake ya kufungiwa michezo mitatu kutarajia kufikia kikomo kesho Jumanne (Februari 15) kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Biashara United Mara utakaounguruma Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mkongomani huyo alifungiwa michezo mitatu na faini baada ya kumpiga kiwiko mchezaji wa Polisi Tanzania, wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Kocha Nabi, amesema ameanza kumuingiza beki huyo katika mipango yake ya mchezo ujao wa ligi baada ya kuikosa michezo miwili huku akisubiria dhidi ya Biashara United Mara ambao atakuwa anamalizia adhabu yake.
Kocha huyo kutoka nchini Tunisia amesema, hivi karibuni alifanya kikao na beki huyo na kumtaka kupunguza jazba za ndani ya uwanja mara baada ya kuchezewa vibaya na wachezaji wa timu pinzani.
“Wachezaji wangu karibia wote wanachezewa vibaya kwa kupaniwa na wachezaji wa timu pinzani, hivyo nisingependa kuwaona wakiwa na jazba mara baada ya kuchezewa vibaya kwa kurudishia.
“Nilishamuonya Djuma kutorudishia rafu atakazokuwa anachezewa na wachezaji pinzani kwa hofu ya kupewa adhabu kama aliyoipata ambayo inaigharimu timu katika kupata matokeo mazuri ya ushindi,” amesema Nabi.
Djuma Shaban tayari ameshakosa michezo miwili dhidi ya Mbao FC (Kombe la Shirikisho), Mbeya City (Ligi Kuu Tanzania Bara) huku mchezo watatu ukitarajiwa kuwa dhidi ya Biashara United Mara (Kombe la Shirikisho).