Beki wa kulia kutoka DR Congo na klabu ya Young Africans Djuma Shabani ni miongoni mwa wachezaji wa klabu hiyo waliosafiri na kufika salama Mkoani Morogoro, tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.
Young Africans itakua Mgeni wa Mtibwa Sugar kesho Jumatano (Februari 23), katika Uwanja wa Manungu Complex Wilayani Mvomero, mchezo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kote.
Djuma anatarajiwa kucheza mchezo huo, baada ya kumaliza adhabu ya kufungiwa michezo mitatu, kufuatia utovu wa nidhamu aliouonyesha wakati wa mpambano dhidi ya Polisi Tanzania uliounguruma Jijini Arusha.
Mbali na Djuma Shabani kusafiri hadi mkoani Morogoro, wachezaji Kibwana Shomari, Yassin Mustapha na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ nao huenda wakacheza dhidi ya Mtibwa Sugar, baada ya kupona majeraha.
Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 36, huku Mtibwa Sugar ikisota katika nafasi 15 ikiwa na alama 12.