Beki wa Kulia wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Djuma Shaban ametamba wataifunga Simba SC keshokutwa Jumapili (April 16), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Miamba hiyo inatarajia kukutana kuanzia saa kumi na moja jioni, huku ikiwa na kumbukumbu ya kuambulia matokeo ya sare ya 1-1 katika mchezo wa Mzunguuko wa kwanza msimu huu 2022/23, mabao hayo yakifungwa na Viungo Augustin Okrah na Stephen Aziz Ki.
Djuma Shaban ambaye alisajiliwa Young Africans msimu uliopita akitokea AS Vita Club ya nchini kwao DR Congo amesema wachezaji wote wa Young Africans wana kila sababu ya kuendeleza ubabe dhidi ya Simba SC, kutokana na timu yao kuwa na uwezo mkubwa wa kupambana.
Amesema wanatambua umuhimu wa mchezo huo, na ndio maana wamejipanga kuhakikisha wanashinda dhidi ya Simba SC, ili kujiongezea matumaini ya kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.
“Timu yetu kwa sasa iko na ubora mkubwa tumekuwa na muendelezo mzuri wa kushinda licha ya mabadiliko ya kikosi chetu, unapopata nafasi lazima ufanye vizuri kwa kuwa kuna wengine nao wanaweza kufanya vizuri siku wakicheza,”
“Hatujashinda ubingwa bado na ili tuchukue taji tunatakiwa kushinda mechi mbili na kuanzia hii ya Simba, hatutakiwa na mchezo hata kidogo, Yanga tutashinda mashabiki wetu waje.” Amesema Djuma Shaban
Hadi sasa Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 68, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 60 huku kila timu ikicheza michezo 25 hadi sasa.