Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa amejitokeza na kukanusha kujihusisha na shughuli yoyote katika mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya kuwepo akaunti inayotoa kauli mbalimbalimbali kwa jina lake.

Akaunti hiyo iliyokuwepo kwa muda mrefu hadi kufikia hatua ya kuaminika na wengi kuwa ni akaunti halisi na kwamba anayeandika ni Dk. Slaa, imetoa kauli mbalimbali hivi karibuni ikiwa ni pamoja na kueleza kuwa anatishiwa maisha na ameamua kuomba msaada wa ulinzi kutoka katika mashirika ya kimataifa.

Dk. Slaa ambaye amepumzishwa na chama chake, aliongea na gazeti la Mwananchi kwa njia ya simu na kueleza kuwa taarifa zote zinazosambazwa kwa jina lake sio za kweli na kwamba hajawahi kuwa na akaunti katika mtandaoo huo wa kijamii.

“Sijawahi kuoperate kitu chochote kwenye mtandao wa twitter, sina akaunti ya Twitter,” alisema Dk. Slaa baada ya kutajiwa jina la akaunti inayotumia jina lake.

Hii sio mara ya kwanza kwa Dk. Slaa kuikana akaunti hiyo ambapo mara ya kwanza alijitokeza katika Jamii Forum nakumtaka anayetumia jina lake kuacha mara moja.

Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema kuwa ana mapango wa kusafiri kwenda ughaibuni na mkewe Josephine Mushumbusi. Ingawa hakuweka wazi nchi anayoenda, Dk. Slaa alisema kuwa yeye na mkewe watarejea nchini baada ya wiki moja.

Hata hivyo Dk. Slaa alikataa kuzungumzia mapumziko yake na uamuzi wa kuwa pembeni ya shughuli za Chadema pamoja na mustakabali wake kisiasa baada ya kutoridhishwa na uamuzi wa chama hicho kumkaribisha Edward Lowassa na kumpa nafasi ya kugombea urais. Aliwataka watanzania kuwa wavumilivu na kwamba muda ukifika atazungumza.

 

 

Ray Awaonya Wasanii Na Siasa Za Tanzania, Awataka Wamchague Huyu..
Tetesi Za Usajili Barani Ulaya