Hatimaye Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson amezungumzia hatima ya mgogoro kati yake na wabunge wa vyama vya upinzani na kueleza kuwa hawawezi kumuondoa katika nafasi hiyo.

Katika mahojiano aliyofanya na Tido Mhando wa Azam TV, Dk. Tulia alisema kuwa kanuni za Bunge zinaruhusu wabunge waliomchagua kumpigia kura ya kumuondoa katika nafasi hiyo, lakini kutokana na idadi ya wabunge wa Ukawa, hawana uwezo wa kufanya hivyo.

“Kwa kuwa waliopeleka hoja ni wabunge wa upinzani, hivyo wanatakiwa kufikisha idadi fulani ambayo kiuhalisia wao kwa sasa hawana,” Dk. Tulia alikaririwa.

Aidha, alisema kuwa hana mpango wa kukaa chini na wabunge wa Ukawa kumaliza tofauti zao kwani hana malumbano nao na kwamba kinachotakiwa sasa ni kusubiri taratibu za kibunge za kanuni baada ya wabunge hao kuwasilisha hoja yao kisheria.

Wabunge wa Ukawa wamekuwa wakitoka Bungeni katika kila kikao kilichokuwa kikongozwa na Dk. Tulia baada ya sala ya asubuhi. Wabunge hao wanampinga Naibu Spika wakidai anavunja kanuni za bunge na kuendesha Bunge kwa kulinda maslahi ya Serikali na kupendelea wabunge wa CCM.

Serikali Yakaribisha Wawekezaji Kutoka India
Mbowe awazuia BAVICHA kwenda Dodoma, aandaa mbinu mpya