Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema kuwa atakayejihusisha na vitendo vya rushwa katika mchakato wa chama hicho tawala kusaka wagombea wake katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, atapoteza sifa za kugombea.
Ameyasema hayo alipokutana na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya za Muleba na Biharamulo mkoani Kagera.
Amesema kuwa kila kiongozi wa CCM atakayejitokeza kugombea uenyekiti wa kijiji au mtaa, lazima awe mwadilifu na mwaminifu, na kuongeza kuwa baadhi ya wagombea wanatumia majukwaa kupinga rushwa licha ya kuwa wanajihusisha nayo, ikiwa ni pamoja na kukiuka maadili ndani ya chama.
“Makatibu wa CCM kila ngazi hata nyie msiwe wa kupokea rushwa kupitisha majina ya wagombea wasiokuwa na sifa lazima kiongozi afuate miiko na ahadi za mwanachama,” amesema Dkt. Bashiru.
Hata hivyo, Dkt. Bashiru yupo katika mapumziko ya mwisho wa mwaka mkoani Kagera ambapo pamoja na mapumziko hayo mafupi, anaendelea na ziara mbalimbali katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.