Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amejibu maelezo ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na kada wa chama hicho, Bernard Membe kuhusu utaratibu wa kumuona.
Membe, kupitia akaunti ambayo inasadikika kuwa ni ya kwake kwenye mitandao ya kijamii, ameeleza kuwa ataenda kumuona Dkt. Bashiru ofisini kwake ingawa alieleza kushangazwa na utaratibu alioutumia kumuita.
“Nimeshangazwa kidogo na utaratibu alioutumia kuniita. Lakini kwasababu ya ugeni kazini, na kwa sababu ninamheshimu nitakwenda kumuona ofisini kwake,” yanasomeka maandishi ya akaunti inayosadikika kuwa ya Membe.
Akizungumza leo na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho wilaya ya Bukombe mkoani Geita, Dkt. Bashiru amesema kuwa hakuna mwanachama yeyote ambaye ni mkubwa zaidi ya chama hicho tawala na kwamba Membe ni mmoja wa wanachama na sio vinginevyo.
“Sikumsema Membe kama mtu maarufu au mtu mwenye nguvu. Nimemsema kama mwanachama wa kawaida, hana tofauti na wanachama walioingia leo. Ila tofauti yake ni kwamba aliwahi kuwa mbunge na waziri,” alisema Dkt. Bashiru.
Alisisitiza kuwa anamhitaji sana Membe, kwani ingawa kumekuwa na chaguzi nyingi ndogo na mikutano kadhaa hajawahi kumuona kada huyo, hatua iliyofanya aeleza kuwa angekuwa na namba yake ya simu angempigia.
Aidha, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa CCM ya sasa ni tofauti na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita, wakati ambapo kwa mujibu wake watu wenye pesa ndio waliokuwa na nguvu ndani ya chama hicho.
Alisema kuwa katika kipindi hicho, chama hicho kilijaa majungu, fitna na uhasama wa makundi, mambo ambayo alisema ni mwiko kwa CCM ya sasa.
Membe alikuwa mmoja kati ya wanachama waliowania nafasi ya kupitishwa na chama hicho kuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka 2015. Alikuwa miongoni mwa wanachama wawili waliokuwa kwenye mchakato waliokuwa na nguvu zaidi kabla ya mchakato, lakini wote hawakufanikiwa kupata nafasi hiyo.