Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amempongeza askari polisi wa mkoani Pwani ambaye siku za hivi karibuni aligoma kutumia salamu ya ‘Kidumu Chama cha Mapinduzi’ inayotumiwa na chama hicho tawala nchini.

Askari huyo aliombwa kutoa salamu hiyo na mjumbe wa halmashauri Kuu Taifa ya chama hicho, Haji Jumaa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Vianzi wilayani Mkuranga, kabla ya kueleza kero za kufungwa kituo cha polisi muda wa kazi.

Dkt. Bashiru ametoa kauli hiyo Jumanne Agosti 27, 2019 katika mkutano wa wanachama wa CCM wilaya ya Ubungo ikiwa ni sehemu ya ziara yake iliyoanza ya kukagua uhai wa chama, miradi ya maendeleo na kuzindua mashina.

Akitolea mfano wa tukio hilo, Dkt. Bashiru amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakiwezi kuwa chombo cha nidhamu kwa watumishi wa umma.

“Nampongeza yule askari aliyegoma kufuata maelekezo nataka nimjue hata IGP nilimpigia simu kuhusu tukio hilo. Polisi hapokei maelekezo ya chama chochote cha siasa iwe CCM au CUF. Kama una jambo usibwatuke tu, sitaki kusikia amri au maelekezo yoyote, tukiendelea na tabia hiyo tutakuwa tunajenga nchi isiyofuata sheria,” amesema Dkt. Bashiru.

Amebainisha kuwa watumishi wa umma wana vyombo vyao vya kuwajibishana na wakati mwingine hupeana adhabu.

Hata hivyo, askari huyo aligoma akisema maadili ya kazi yake hayaruhusu kutoa salamu hiyo, akidai ni kosa kimaadili.

 

Rais Museveni adai hana mpango wa kustaafu mapema
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 28, 2019