Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. Bashiru Ally, ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuwapuuza wale watu wanaoendeleza mjadala usiokuwa na tija ndani ya chama hicho, na akawahakikishia kwamba chama hicho kiko imara.

Dk. Bashiru  ameyasema hayo wakati akitoa pongezi kwa hatua ya wanaCCM Mkoa wa Dodoma, kutaka Kanali Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, makatibu wastaafu wa CCM kuchukuliwa hatua.

Makatibu hao wastaafu wiki iliyopita, walimwandikia barua Pius Msekwa, Katibu wa Baraza la Viongozi Wastaafu wa CCM wakilalamikia kuchafuliwa na Cyprian Musiba, anayejitambulisha kuwa mtetezi wa Rais John Magufuli.

Kwenye barua hiyo, Makamba na Kinana wamelalamika kuchafuliwa na kuzushiwa huku wakidai serikali imeshindwa kuchukua hatua na kuhoji ulinzi ulinzi anaopewa mtu huyo anayewachafua.

“Wapuuzeni, hatuogopi kukosolewa, lakini hatuko tayari kudharauliwa, kutukanwa na kubezwa na majina yaliyo na kebehi na watu wasio na shukrani, hatujafunzwa hivyo, hatujazoea hivyo,” amesema Dkt. Bashiru

Aidha, amesema kuwa uongozi wa CCM hautaruhusu malumbano ndani ya chama hicho, huku akieleza kwamba mwenyekiti wake, Dkt. Magufuli yuko tayari kuwasamehe, ili kukijenga chama.

“Msijifanye majasiri wa kupambana na malumbano, hakuna ruksa hiyo kwenye chama chetu. Waacheni waseme watakachotaka wenyewe. na ole wake mwanaCCM yeyote atakayetaka kutumia fursa ya malumbano hayo kutafuta kiki, ya kisisasa ili achaguliwe kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, hapana msifanye hivyo.

“Jifunzeni kutoka kwa kiongozi wetu ambaye wakati wote hana muda wa malumbano. amevumilia, wanaomtusi wengine wana umri wa watoto wake amewavumilia na yuko tayari kuwasamehe pia.  Lakini kwa kufanya hivyo si kwamba ni muoga,”ameongeza Dkt. Bashiru

 

LIVE IKULU: Makabidhiano ya Dhahabu iliyokamatwa nchini Kenya inawasilishwa na Mjumbe wa Rais Kenyatta
Waziri wa afya ajiuzulu, amtupia dongo Rais