Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Bashiru Ally amempongeza mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya kuwa ni mbunge mahiri, makini na mchapakazi ndiyo sababu wakakubali kumpokea ndani ya chama hicho, kwani waliwakataa wabunge watatu wa vyama vya upinzani ambao waliomba kujiunga na CCM baada ya kubaini kuwa hawawezi kukidhi vigezo vya kuwa wabunge wa chama hicho.
 
Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika Mji mdogo wa Orkesumet Wilayani Simanjiro kwenye ziara yake ya siku mbili Mkoani Manyara, ambapo amesema kuwa Ole Millya ni miongoni mwa wabunge 10 mahiri waliokuwa upinzani wakakubaliwa kujiunga na CCM.
 
Amesema kuwa kwenye mkoa wa Manyara waliwapokea viongozi wawili wa upinzani Ole Millya na Pauline Gekul wa jimbo la Babati Mjini ambaye alikuwa mwanafunzi wake chuo kikuu.
 
“Tumewakataa wabunge hao watatu waliotaka kuja kwetu kwani CCM siyo jalala, mtu aliyekata tamaa anaweza kujiumiza mwenyewe au kuumiza wenzake,” amesema Dkt. Bashiru
 
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Simanjiro, James Ole Millya amesema kuwa miradi mingi ya maendeleo iliyofanyika Wilayani Simanjiro kupitia Rais Dkt. John Magufuli ndiyo sababu ya yeye akajiuzulu Chadema na kujiunga na CCM.
Pia ameongeza kuwa hivi sasa hospitali ya Wilaya inajengwa, mradi mkubwa wa maji wa Mto Ruvu, Barabara ya Lami itajengwa kutoka Arusha hadi Kongwa Mkoani Dodoma kupitia Simanjiro na Kiteto na Ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite katika Mji mdogo wa Mirerani.
 
Naye Mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Manyara, Simon Lulu amesema kuwa hivi sasa majimbo yote saba ya mkoa huo yanaongozwa na wabunge wa CCM na Halmashauri zote saba zinaongozwa na wenyeviti kupitia CCM

LIVE CHATO: Rais Magufuli akiagana na rais wa Uganda, Yoweri Museveni
Utalii wa Sokwemtu kuanzishwa katika hifadhi ya Rumanyika