Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka Watendaji na Watumishi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA, kuzingatia maslahi ya Watanzania na maslahi ya nchi katika kazi zao za Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ili Watanzania wapate huduma bora na kwa unafuu mkubwa.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akifungua Kikao cha Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika hii leo Novemba 8, 2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa, Rugemalira Rutatinwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Bi. Ziana Mlawa.
Amesema, “tambueni kuwa Taifa lina mategemeno makubwa na ninyi, hivyo fanyeni kazi zenu kwa weledi na ubunifu mkubwa unaoendana na kasi ya teknolojia na maendeleo ya dunia; kanuni na miongozo yenu mnayotumia katika utekelezaji wa majukumu iundwe katika mifumo rafiki kulingana na hali iliyopo ili ilenge kuleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa na hivyo Watanzania waendelee kupata huduma bora na kwa gharama stahiki.”
Dkt. Biteko pia amewataka Watumishi wa EWURA kuweka mkazo kwenye kudhibiti vitendo vya urasimu na rushwa mahali pa kazi, kutoangalia maslahi binafsi wakati wa kutenda kazi ili kuepusha kuwaumiza Watanzania walio wengi, na ametoa wito kwa wafanyakazi hao kumkemea mtu yeyote anayeonekana kuwa na vitendo vya rushwa na ubinafsi katika eneo la kazi.
Aidha, amewasisitiza Wafanyakazi wa EWURA kuwajibika ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao kwa kuhakikisha kuwa Watoa Huduma wanafanya ushindani wenye tija na ufanisi wa kiuchumi, kulinda maslahi ya Walaji na mitaji ya kifedha ya Watoa Huduma pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma kwa makundi yote ikiwemo ya watu wanaoishi vijijini.