Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameungana na Viongozi mbalimbali wa kitaifa na Watanzania kwa kutoa salamu za pole kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kufuatia kifo cha Kaka yake, marehemu Issa Juma, aliyezikwa leo.
Akizungumza leo Novemba 6, 2023 Wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi wakati akitoa salamu hizo kwa niaba ya Mawaziri, Dkt. Biteko amesema watanzania wanaupendo wa dhati kwa Waziri Mkuu Majaliwa ambao wameuonesha pia katika kipindi hichi cha kumpoteza marehemu kaka yake.
“Sisi ni kielelezo kuwa Watanzania wanaupendo nawe ndio maana tumekuja kuungana pamoja na wewe, kulia pamoja na wewe lakini kukutia moyo kwamba sisi tuliofika hapa na wengine tunakupa pole kwa msiba wa kumpoteza kaka,” ameeleza Dkt. Biteko.
Amesema kuwa, jambo lolote linalotokea ni mipango ya Mwenyezi Mungu hivyo ni muhimu kuombeana heri ili tuwe na mwisho mwema duniani.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewashukuru Watanzania kwa kumfariji katika kipindi hichi cha msiba wa kaka yake. Amesema amepokea salamu za pole kutoka kwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Mwinyi na watanzania wote wanaompa pole na kumfariji.
Naye, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson akiwasilisha salamu kwa niaba ya Wabunge, ametoa pole kwa Waziri Mkuu Majaliwa na familia yote kwa kuondokewa na mpendwa wao na kusisitiza kuendelea kushirikiana na kutenda mazuri yanayompendeza Mungu.
Wengine walioshiriki kumpa pole Waziri Mkuu ni Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa ya Lindi na Mtwara, Wakuu wa Wilaya, Vyama vya Siasa na Wananchi wa Mkoa huo.