Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo Oktoba 31, 2023 amewasilisha azimio la kujiunga na Mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (Statute of the International Renewable Energy Agency – IRENA), Bungeni jijini Dodoma.
Dkt. Biteko ametaja manufaa mbalimbali yatakayopatikana baada ya kujiunga na mkataba huo ikiwemo kuimarika kwa mchango wa Nishati Jadidifu, katika uzalishaji wa Nishati ya Umeme nchini na kuliwezesha Taifa kuwa na vyanzo mchanyanyiko vya umeme, unaoendana na mahitaji ya ukuaji wa kiuchumi na kijamii.
Ameyataja manufaa mengine kuwa ni kuimarika kwa uwekezaji, mitaji na upatikanaji wa ushauri wa kiufundi katika uendelezaji wa nishati jadidifu na kupungua kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji na matumizi ya nishati isiyo rafiki wa mazingira na pia kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mapema hapo jana Oktoba 30, 2023 Dkt. Doto Biteko alifunga Semina ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, ambayo ililenga kuwapa uelewa Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu Mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (IRENA), ambapo Tanzania imeonesha nia kujiunga na mkataba huo kutokana na faida zake.