Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameagiza kuundwa kwa Kamati Maalum ya Wataalamu ili kuchunguza uwepo wa milipuko inayolalamikiwa na wananchi kuwa chanzo cha mitetemo wanayoipata katika eneo la Kijiji cha Ulowa kilichopo Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga.
Dkt.Biteko ametoa agizo hilo leo Aprili 30, 2022 katika Kijiji cha Ulowa Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama Mkoa wa Shinyanga na kutaka kazi hiyo ifanyike ndani ya wiki mbili.
Dkt. Biteko amesema, Wizara ya Madini kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) itapeleka timu ya wataalamu inayohusika na mitetemo ya ardhi ambayo watafanya kazi ya uchunguzi kwa muda wa wiki mbili.
Amesisitiza kuwa, tetemeko la ardhi haliwezi kuwa limesababishwa na shughuli za kibinadamu kwa kuwa hakuna ulipuzi wa miamba mikubwa unaofanyika katika eneo hilo.
Amesema GST itasimika kifaa maalum katika eneo la Ulowa kwa ajili ya kunakili mawimbi ya mitetemo mbalimbali itakayotokea katika eneo hilo ili kupata taarifa sahihi juu ya chanzo halisi cha mitetemo hiyo.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojojia na Utafiti wa Madini Tanzania, Dkt. Musa Budeba amesema, GST itafanya utafiti wa ziada ili kubaini chanzo cha mitetemo katika maeneo hayo na kusisitiza kuwa wataalamu watafika katika maeneo ya mitetemo ili kuondoa hofu walizonazo wananchi hao kuhusu matetemeko ya ardhi.
Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi, John Kalimenze akisoma taarifa kuhusu mitetemo ya ardhi inayosadikiwa kuwa tetemeko la ardhi amesema, jumla ya wananchi takribani mia moja walipatiwa elimu na mafunzo kuhusu tetemeko la ardhi, namna gani linatokea, jinsi ya kuchukua tahadhari kabla halijatokea, wakati linapotokea na baada ya kutokea.
“Mafunzo hayo yalisaidia sana kupunguza taharuki iliyokuwepo miongoni mwa wakazi wa Ulowa namba 8 na maeneo ya jirani kama ambavyo waliwaeleza wataalamu baada ya kupatiwa mafunzo,” amesema Kalimenze.
Taarifa za mitetemo kutoka Kituo cha GST cha kuratibu mitetemo ya ardhi kilichopo mjini Geita zinaonesha kwamba, hakuna matetemeko ya ardhi yaliyotokea katika eneo la Ulowa katika kipindi cha tarehe 19 hadi 21 Aprili, 2022 kama ilivyodaiwa na wananchi wa Ulowa.
Kikao hicho, kimehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani, Diwani wa Kata ya Nyamilangano, Robert Mihayo na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Madini na Tume ya Madini.