Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana amezitembelea ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) zilizopo mkoani Morogoro.
Akizungumza na menejimenti na watumishi wa TAWA Waziri Chana amesema ziara hiyo imelenga kufahamu majukumu ya TAWA kama moja ya Taasisi zilizopo chini ya Wizara yake, kujitambulisha na kuzungumza na watumishi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu TAWA.
Waziri Dkt. Chana amemshukuru rais Samia kwa jitihada zake za kuinua sekta ya utalii nchini ikiwemo uzinduzi wa filamu maalumu ya “Royal Tour” iliyolenga kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini.
Aidha ameagiza Menejimenti na watumishi wa TAWA kuwa tayari kupokea wageni watakaokuja nchini kama matokeo ya filamu ya “Royal Tour”.
“Tuiweke ajenda ya Royal Tour mezani na tuendelee kupanga mikakati ya kupokea wageni hao,” amesema.
Kadhalika, Waziri huyo amewapongeza watumishi wa TAWA kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhifadhi rasilimali za Maliasili kote nchini.
Ametoa wito kwa kila mtumishi kuendelea kuwa mfano bora kwenye eneo lake la kazi ili kuendelea kuipa heshima Tanzania kimataifa.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali (Mstaafu) Hamis Semfuko, amemuahidi Balozi Dkt. Chana kuwa TAWA wataendelea kutoa ushirikiano mkubwa, kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa bidii.
Awali, akitoa taarifa ya utendaji kazi ya TAWA, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi- TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, amesema TAWA imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kusaidia kupungua kwa shughuli za ujangili, kuimarika kwa shughuli za uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada wa kielektroniki na uboreshaji wa miundombinu ya utalii kwenye maeneo ya hifadhi.