Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya ufuatiliaji wa maelekezo yake katika kuboresha huduma za matibabu kwa Wazee kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri Dkt. Dorothy Gwajima alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma na kujionea jinsi walivyoweza kutekeleza maagizo ya utoaji wa huduma za afya kwa Wazee wanaofika kupata matibabu Hospitalini hapo.

Dkt. Gwajima amesema mahitaji ya maboresho ni mengi hivyo wizara yake imeona ianze na vile ambavyo Wazee wamekuwa wakivilalamikia kila siku ikiwemo mapokezi yasiyoeleweka na kutopata huduma iliyokusudiwa.

“Kila kituo lazima kiwe na nesi mmoja, afisa ustawi wa jamii pamoja na daktari aliyepangwa zamu na lazima wavae sare ambayo itamtambulisha na imeandikwa ‘Mzee ni Tunu, Tunakupenda, Tunakuheshimu’ pamoja na kuweka mabango yanayomuelekeza au kumuongoza Mzee wapi atapata huduma anazozihitaji na ambayo yameandikwa ‘Mpishe Mzee apate huduma kwanza,” amesema Gwajima.

Dkt. Gwajima amesema wametoa maelekezo hayo katika Hospitali na vituo vya afya vyote na kwa hatua hiyo sasa Wizara inaenda kutengeneza muongozo ambao utakua wa uwiano kwa Hospitali zote.

Aidha, ameipongeza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Dodoma kwa kuanza utekelezaji huo.

Safari ya Mukoko kwenda Horoya FC iko hivi
Dangote kuineemesha Tanzania