Katibu wa NEC Uchumi na Fedha wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni mlezi wa chama hicho mkoa wa Njombe Dkt. Frank Hawasi amepokea wanachama wapya zaidi ya 115 waliojiunga na chama hicho katika tawi la Lunguya Kata ya Mtwango Mkoani Njombe.
Dkt. Hawasi amefungua Shina jipya la wakereketwa katika tawi la Lunguya lenye wanachama 43 ambapo wamefanikiwa kujenga kituo maalumu kwa ajili ya kukutana na kufanya mikutano yao ya chama.
Amesema kuwa jukumu kubwa la chama cha mapinduzi kote nchini ni kushughulika na shida za watu ambao chama kina waongoza kupitia serikali yake iliyoko madarakani chini ya Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
‘’Nawapongeza sana kwa uamuzi huu mliouchukua wa kuamua kujenga kituo hiki kwaajili ya kuzidi kukitangaza chama naona jinsi gani watu wa Lunguya mmeamua kukiamini chama hiki ambacho kimeendelea kushughulika na shida za watu popote nchini,’’amesema Dkt. Hawasi
Hata hivyo, Dkt. Hawasi anaendelea na ziara yake katika wilaya ya Wanging’ombe Mkoani humo kwa lengo la kutoa pole kwa wananchi kufuatia mauaji ya watoto wadogo yaliyotokea mkoani Njombe na kujitambulisha kwa wanachama kama mlezi wa mkoa huo pamoja na kuzidi kuimarisha chama.