Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira – NEMC, kwa utekelezaji wa majukumu yake.
Jafo ametoa pongezi wakati akizungumza kwenye kikao cha 16 cha Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya NEMC kilichofanyika jijini Dodoma.
Amesifu utaratibu wa kutembelea maeneo mbalimbali kukagua shughuli za kulinda mazingira hususan katika migodi iliyopo ya mkoani Geita na kwengineko.
Aidha, ametoa rai kwa Bodi hiyo kuendelea kuisimamia NEMC inapotekeleza Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 katika maeneo mbalimbali na kuwachukulia hatua wanaoikiuka.
Jafo amesema ni jukumu la NEMC kuhakikisha wenye viwanda, migodi na maeneo ya starehe yanafuata sheria ili kudhibiti changamoto za uchafuzi wa mazingira zikiwemo utiririshaji wa majitaka, moshi au kelele na mitetemo.