Wakati dunia ikiwa kwenye taharuki kubwa ikihofia kutokea vita kamili kati ya Iran na Marekani iliyochochewa na hatua ya Marekani kumuua Kamanda wa Iran, Qassem Soleimani, mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Dkt. Charles Kayoka ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amefichua yaliyofichika kwenye taharuki hiyo.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Dar24 Media, Dkt. Kayoka amesema kuwa hatua ya Marekani kumuua kamanda Soleimani kwa madai kuwa alikuwa gaidi ni ‘kichekesho’, kwani wamewahi kushirikiana nao kupambana na makundi ya kigaidi Mashariki ya Kati.

Dkt. Kayoka amesema kuwa Soleimani ndiye aliyefanya kazi kubwa ya kupambana na kundi la Islamic State of Iran and Syria (ISIS), pamoja na kazi aliyowahi kufanya ya kupambana na kundil la Taliban chini Afghanistan kwa lengo la kuleta amani katika ukanda huo.

“Nimesema ni kichekesho kwa sababu, mwaka 2003, majeshi ya Iran yakiongozwa na Soleimani yalikuwa yanapigana kwa kushirikiana na Marekani Afghanistan dhidi ya Taliban. Kwa sababu Taliban walionesha kabisa kwamba wale ni watu wanaoeneza siasa kali na kuleta vurugu katika ukanda wa Mashariki ya Kati. Rais wa wakati ule wa Iran aliruhusu waende wakaisaidie Marekani kuipiga Taliban,” amesema Dkt. Kayoka.

“Lakini George Bush [aliyekuwa Rais wa Marekani], alienda hadharani na kutangaza kuwa Iran ni moja kati ya nchi ambazo ni mihimili ya siasa kali na ugaidi, hapo Kamanda Soleimani akaamua kuondoka, na alipoondoka tunaona mpaka sasa Taliban bado ipo. Akiwa ameshiriki alisaidia sana kuipunguza nguvu Taliban. Kwahiyo, inaonekana Marekani hawataki kuwe na amani Afghanistan ili waendelea kujinufaisha,” ameongeza.

Mhadhiri huyo ameeleza kuwa Ushiriki wa Kamanda Soleimani katika kupambana na ISIS nchini Iraq na Syria kulisaidia kulizuia kundi hilo kulichukua jiji la Baghdad.

Akizungumza saa chache baada ya kumuua Soleimani kwa agizo lake, Rais Trump alimtaja kuwa ni gaidi ambaye mikono yake imejaa damu za watu wa Iran na Marekani.

Iran wameapa kulipa kisasi na juzi walishambulia kambi mbili za kijeshi za Marekani zilizoko nchini Iraq. Kwa mujibu wa Iran waliwaua wanajeshi 80 wa Marekani, lakini Rais Trump ameeleza kuwa hakuna aliyepoteza maisha na hakukuwa na majeruhi.

Akizungumzia uwezekano wa kuwepo Vita Kuu ya Tatu ya Dunia kutokana na mgogoro huo, Dkt. Kayoka ameeleza kuwa hakuna uwezekano huo kwa asilimia kubwa kwakuwa nchi nyingine kubwa zinazoweza kujiunga na vita zisingependa kujiunga kutokana na madhara makubwa yanayoweza kutokea.

Aidha, ameeleza kuwa Trump anapenda amani lakini walionyuma yake ambao kwa kiasi kikubwa ni Wayahudi wa Israel ndio wanaomshinikiza kupambana na Iran.

Pia, amesema endapo kutatokea vita hiyo, nchi za Afrika pia zitaathirika kwa kiasi kikubwa kwakuwa mataifa hayo yatabadilisha vipaumbele na kuacha kutoa misaada na miradi mbalimbali ya maendeleo katika nchi hizo, ili waweza kumudu gharama kubwa za vita.

Haya hapa matokeo kidato cha nne, kidato cha pili na darasa la nne
NECTA yafuta matokeo ya watahiniwa 333