Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt Ashatu Kijaji amesema kuwa bendera ya Tanzania kupandishwa kwenye jengo refu zaidi duniani la Burj Khalifa jijini Dubai ni zawadi kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Taifa.

Leo Jumatano Machi 2, 2022 Dkt Kijaji wakati akizungumzia mafanikio ya ziara ya Rais Samia aliyoifanya katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) katika majadiliano kupitia mtandao pamoja na viongozi wengine wa serikali.

Amesema kuwa bendera hiyo ambayo ilipandishwa kwenye jengo refu kuliko yote duniani ilipandishwa usiku wa kuamkia Jumanne ikiwa ni kuitangaza Tanzania na fursa zinazopatikana na hiyo ni moja ya mafanikio ya ziara hiyo.

“Wote tumeona kilichotokea kule Jiji la Dubai, kuonyesha umuhimu wa ziara ya Rais aliyoifanya, ndani ya Jiji la Dubai walionyesha bendera ya Tanzania kwenye jengo kubwa zaidi duniani kama zawadi kwa Rais na Taifa letu,” amesema Dkt Kijaji

Amesema kuwa siku moja baada ya kupandishwa bendera hiyo, usiku uliofuatia ilipandishwa tena pamoja na picha ya Rais Samia.

“Jana tena usiku wakarusha bendera ya Taifa letu ikiwa na picha ya Rais wetu hasa tukiwa kwenye mwezi huu wa tatu ambao tunasherekea malkia wa nguvu pote duniani na Tanzania tukiongozwa na malkia wa nguvu mama yetu Samia,” amesema.

Amesema kuwa hiyo moja ya njia ya kuonyesha na kutangaza fursa zinazopatikana Tanzania na kuwataka Watanzania kutarajia kuendelea kuona fursa zikiendelea kutangazwa kwenye jengo hilo.

“Katika kuendelea kuitangaza na kuuza fursa tulizonazo, Watanzania watarajie siku ya leo wataona pia bendera yetu ikiendelea kupandishwa kwenye jengo lilelile na leo hii tutakuwa na picha ya Mlima Kilimanjaro.” amesema Dkt Kijaji.

Amesema hizo ni jitihada za kuitangaza Tanzania kwa wawekezaji kuwa nchi iko salama na ina fursa nyingi za uwekezaji na itafanyika kwa mwezi mzima.

Juzi, ilisambaa video kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha bendera ya Tanzania ikiwa imefunika jengo hilo refu duniani lililopo Dubai.

Waliokuwa wafungwa wafunga ndoa gerezani
Biden:"Putin alikosea"