Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – UDSM, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema amefurahishwa kuona asilimia ya wahitimu wanawake chuoni hapo imefikia asilimia 54.7 na kuwashauri wanafunzi wanaume wafanye juhudi ili wasiachwe mbali sana na wenzao.
Akiongea kabla ya kuhitimisha Duru la Pili la Mahafali ya 53 ya chuo hicho, Dkt. Kikwete amesema amefurahishwa kuona Wanawake “wakiupiga mwingi” na kuwataka vijana wa kiume walichukulie jambo hilo kama changamoto kwa wao kufanya vizuri zaidi kwenye masomo.
Katika mahafali hayo yalifofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, jumla ya wahitimu 2796 walihudhurishwa ikiwa ambapo 2700 walitunukiwa Shahada za Awali ikiwa ni wasichana 1488 na wavulana 1212 na Stashahada 78 zilitolewa kwa wanaume 45 na Wasichana 33, wakati wanaume 10 na wasichana wanane walitunukiwa Astashahada.
Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Anangisye aliwapongeza wahitimu wote huku akiwashauri watumie elimu waliyopata kuleta ushawishi chanya, kwa watu wote wanaowazunguka na kuwa chachu ya mabadiliko katika jamii.