Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania, Jakaya Nrisho Kikwete amesema amani na usalama ni maneno yenye dhana pana tofauti na watu wengi wanavyoelewa kuwa ni huru na migogoro inayotumia silaha, kauli ambayo ameitoa Agosti 12, 2023 wakati akiwasilisha mada, kuhusu Amani na Usalama, kama kigezo cha msingi cha kufikia maendeleo ya kweli ya eneo la Kusini mwa Afrika.
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jopo la Wazee wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC, aliwasilisha mada hiyo kwenye Chuo cha Diplomasia cha Angola wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC ulioanza Agosti 8, 2023 kwa ngazi ya Maafisa Waandamizi na Utahitimishwa na Mkutano wa Marais utakaofanyika tarehe Agosti 17, 2023.
Dkt. Jakaya Kikwete (katikati), wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Amani na Usalama kama msingi wa kufikia maendeleo ya kweli katika nchi za Kusini mwa Afrika – SADC. Kulia ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Msumbiji, Luisa Diogo na Katibu Mtendaji wa Zamani wa SADC, Tomaz Salomão.
Amesema, “Amani na Usalama ni dhana pana inayojumuisha mambo mengi kama vile elimu, afya na ustawi wa jamii, pia ni msingi wa maendeleo Kusini mwa Afrika na itakapokosekana mahali popote pale, watu wasitarajie kupata maendeleo.”
Aidha, Dkt. Kikwete alitoa mfano wa nchi zilizokuwa na migogoro ya kisiasa kwa muda mrefu kama Angola na Msumbiji namna zilivyoathirika kiuchumi hadi pale ufumbuzi ulipopatikana na kudai kuwa utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani na mazingira tulivu yaliyopo hivi sasa, imeshuhudiwa kwa mataifa mengi ya kusini mwa Afrika huku yakipiga hatua za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Sehemu ya Washiriki wakisikiliza mada kuhusu Amani na Usalama kama msingi wa kufikia maendeleo ya kweli katika nchi za Kusini mwa Afrika – SADC, iliyokuwa ikiwasilishwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Aliongeza kuwa, Taifa lisilokuwa na amani haliwezi kufanya biashara, kuvutia uwekezaji kutoka nje na ndani, kujenga miundombinu kama Barabara, shule na Vituo vya Afya kwani fedha zote ambazo Serikali inazipata, zinatumika kununua silaha kwa ajili ya kujilinda.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kushirikiana na kuhamasisha amani katika nchi zao, akisema itaziwezesha Serikali za nchi hizo kujiamini na hatimaye kuwa na utawala bora, utawala wa sheria na kutoa haki kwa watu wote.
Viongozi wengine mashuhuri walioungana na Kikwete kuwasilisha mada katika Mhadhara huo wa Umma ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Msumbiji, Luisa Diogo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zamani wa Angola, Balozi Joao Bernardo de Miranda, na zao zilihusu miundombinu inayohitajika kuunganisha nchi za SADC, hali ya sasa ya Dunia na athari zake.