Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete ametoa rai kwa wadau na viongozi ambao wametokea katika chimbuko la  shule ya Sekondari ya Kibaha, kuangalia namna ya kutatua changamoto ya uhaba wa madarasa ambayo inasababisha mlundikano wa wanafunzi madarasani.

Amesema mbegu ya kuwa yeye mwanasiasa ilipandwa shuleni hapo, baada ya kuchaguliwa kiongozi wa baraza la shule kutokana na harakati zake za kutetea haki za wanafunzi .

Dkt. Kikwete amesema hayo wakati wa mahafali ya 50 ya wanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Kibaha ambako alipata elimu yake ya sekondari mwaka 1966 hadi 1969.

Amesema kuwa atashirikiana na wadau mbalimbali kuona namna bora ya kusaidia kupunguza ama kuondoa tatizo la upungufu wa madarasa, kwani haipendezi na hajafurahishwa na hali ya miundombinu ilivyokuwa chakavu hali inayoathiri mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji .

Dkt. Kikwete amesema kuwa changamoto hizo si sababu ya kushindwa bali  uwepo wa changamoto huongeza umakini ,bidii na ubunifu ili kukabiliana nazo .

Aidha, ameeleza kufurahishwa kusikia Serikali imejizatiti kukarabati shule kongwe nchini na shule ya sekondari Kibaha ikiwemo, hivyo aliwaomba wavute subira maana kulingana na kasi ya awamu ya tano anaamini ukarabati huo hautachelea .

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu shule hiyo, Chrisdom Ambilikile amesema shule hiyo ipo vizuri kitaaluma ambapo imekuwa ikifanya vizuri miaka 13 mfululizo sasa .

Amesema mwaka jana walipanda ufalu kitaifa kufikia nafasi ya 16 kutoka ya 69 hivyo wanatarajia kupanda zaidi .

Aidha, amesema kuwa wanatatizo la upungufu wa madarasa matano, ambao unasababisha mlundikano wa wanafunzi katika vyumba vichache vilivyopo .

Shule ya sekondari ya Kibaha ilianzishwa mwaka 1965 kwa msaada wa kifedha wa nchi za Nordic ikiwa na wanafunzi 110, kwa sasa ina wanafunzi 728 wote wakiume, walimu 57, na wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne  mwaka huu  ni 116.


Video: HATARI!! “Tulivunja shule baada ya kukosa hela, wazazi wangu walinifanyia kitu cha ajabu sana”.

Magazeti ya Tanzania leo Oktoba 2, 2017
Mwinyi atoa neno kwa vijana kuhusu wazee