Waumini wa Dini ya Kikristo Mkoani Njombe wametakiwa kuwa na moyo wa kujitoa na kumtumikia Mwenyezi Mungu ikiwa ni pamoja na kutoa michango yao kwaajili ya kuboresha Miundombinu ya Makanisa.
Hayo yamesemwa na Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe Dkt, Susan Kolimba wakati akizindua Albamu ya nyimbo za Injili iitwayo IMBENI BILA KUCHOKA iliyoimbwa na Kwaya ya Mt, Andrea Parokia ya Uhepela Jimbo Katoliki la Njombe.
Akizindua Albamu hiyo pamoja na kuendesha Harambee ya Ujenzi wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Uhepela iliyopo Kijiji cha Igagala Kata ya Ulembwe Wilaya ya Wanging’ombe, Dkt. Kolimba ametoa Fedha kiasi cha Tsh, 100,000/= kwaajili ya Ufunguzi huo.
“Kutoa ni Moyo wala si utajiri tunatakiwa tumtukuze Mwenyezi Mungu na kumtolea Sadaka kwa moyo mmoja na upendo ili kujenga Makanisa ambayo ni nyumba yake, kwakufanya hivyo naamini tutabarikiwa,” amesema Dkt, Susan Kolimba.
Aidha, Dkt, Kolimba ameipongeza Kwaya ya Mt. Andrea kwa kuamua kufanya kazi ya kutangaza neno la Mungu katika Jamii huku akitoa Fedha kiasi cha Tsh, 800,000/= kwaajili ya kuiunga mkono kwaya hiyo ili iweze kujiboresha kiuchumi.
Mbunge huyo ameahidi kupeleka mifuko 100 ya Saruji kanisani hapo yenye thamani ya Tsh, 1,600,000/= kwaajili ya kuunga mkono juhudi za Waumini wa Kanisa hilo ambao wanaendelea kushiriki ujenzi wa Parokia yao.
Pamoja na Dkt, Kolimba Viongozi wa ngazi mbalimbali walishiriki tukio hilo akiwemo Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Njombe, Rosemary Lwiva na Diwani Viti Maalumu Tarafa ya Imalinyi, Victoria Mbiduka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Parokia ya Uhepela.