Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe, Dkt. Paul Lawala ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya Afya ya akili Nchini inayoendelea kuhamasisha mtu mmoja mmoja kujua na kuchukua taadhari juu ya Afya ya akili.
Akizungumza na Dar24 Media jijini Dodoma hii leo Septemba 8, 2023 Dkt. Lawala amesema tayari wamekutana na wadau wa taasisi mbalimbali ili kujadili namna ya kuongeza nguvu kitendo ambacho kitasaidia kupunguzia muda wa wa Mgonjwa kurudi kwenye hali yake ya kawaida.
Amesema, “tumekutana na wadau wa Taasisi mbalimbali jijini Dodoma kwa lengo la kujadili ili kuongeza nguvu katika afya ya akili na kuendelea kuhamasisha uchukuaji wa taadhari juu ya Afya ya akili, hii itasaidia kutupunguzia muda wa Mgonjwa kurudi kwenye hali yake ya kawaida na wadau ndio watatusaidia kulifanikisha hili.”
Kwa upande wake Afisa Polisi Kata ya Hazina Dodoma, Verediana Mlimba amesema uhalifu unaanza na akili hivyo Polisi wapo pamoja katika kutoa elimu juu ya Afya ya Akili na kuongeza kuwa, “Wadau wote wa Afya ya Akili ni Maaskari Kanzu na mnatusaidia katika kuendelea kutatua changamoto ya Afya ya akili kuanzia Vijijini na Mijini.”
Amesema, “tupo pamoja na ninyi katika kuhakikisha afya ya akili inapewa kipaumbele kuanzia shule za Msingi na Sekondari, pia kufikia vyuo vikuu. Taasisi nyingi zimeshaanza kuwafikia vyuo Vikuu Nchini, niwapongeze wadau wote wa afya ya Akili katika kuendeleza programu hizi za utoaji elimu.”