Tanzania imepata pigo kubwa la kuondokewa na mmoja kati ya wadau wakubwa wa uchumi, maendeleo na falsafa za kizalendo, Dkt. Reginald Abraham Mengi, aliyetangulia mbele ya haki leo, Mei 2, 2019, Dubai alipokuwa mapumzikoni.
Dkt. Mengi ameacha alama zisizofutika katika maisha ya watu wengi na wengine wamefaidika na matunda ya kazi yake kwa njia ambayo sio ya moja kwa moja. Alikuwa mmoja kati ya watoto saba wa mzee Abraham Mengi na mkewe Ndeekyo. Alizaliwa mwaka 1944, Machame mkoani Kilimanjaro.
Alikuwa mfanyabiashara maarufu aliyehesabiwa kati ya matajiri wakubwa zaidi Afrika. Alikuwa Mwenyekiti wa Masharika mbalimbali ikiwa ni pamoja na Shirikisho la Viwanda vya Tanzania, IPP Gold Ltd., Media Owners Association of Tanzania, IPP Ltd na Handeni Gold.
Sehemu ya urithi aliouacha ni ni kitabu ambacho pamoja na mambo mengine kimeelezea wasifu wake ikiwamo safari yake ya maisha ya dhiki akiwa mtoto hadi kuwa msomi mkubwa katika fani ya uhasibu na kisha tajiri.
‘I Can, I Must, I Will, The spirit of success’ ni urithi mkubwa kwa kila atakayesoma kwani ndani ya kitabu hicho ameelezea maisha ya kubangaiza waliyokuwa wakiishi wazazi wake katika vibanda vya udongo katika kijiji cha Nkuu mkoani Kilimanjaro.
Katika kitabu hicho, Dkt. Mengi amesimulia jinsi familia yao ilivyokuwa masikini sana kiasi cha kuishi kwenye vibanda pamoja na ng’ombe, kuku wachache waliokuwa nao.
Alitembea peku kutokana na umasikini, lakini maono ya upambanaji kuufikia utajiri yalisukuma safari yake bila kujali kipindi wanachopitia wakati huo.
“Ninaporudisha fikra na kutazama nyuma ni vigumu napatwa na ugumu wa kufikiri namna tulivyoweza kuishi katika hali ile. Tuliishi kwenye vibanda vya udongo tukichanganyika na ng’ombe na kuku. Familia yetu ilikuwa masikini sana, kila siku ilikuwa ni vita ya kupambana na umasikini,” alisema Dkt. Mengi.
Katika miaka ya 1983, Dkt. Mengi aliona fursa kutokana na uhaba wa kalamu za wino nchini ambazo zilikuwa zikiagizwa kutoka nje, wakati huo kaka yake Elitira kutokana na ugumu wa maisha alikuwa anafanya biashara ya kuuza mayai akiwa bado mwanafunzi wa shule ya msingi.
Kutokana na mbinu za kaka yake alipewa kipawa cha kugundua fursa na kuzigeuza kuwa biashara katika ujasiriamali, zikamvutia Dkt. Mengi, naye akaanza biashara aliyoiona ya kalamu za wino.
Dkt. Mengi alingia katika ulimwengu wa biashara akianza na utengenezaji wa kalamu alizozipa jina la ‘Epica’ kwa kuagiza vifaa kutoka Mombasa akiwa hana mtaji wowote bali kwa makubaliano ya kulipa baada ya mauzo.
Mengi alizidi kutanua wigo wa biashara kadiri siku zilivyokwenda kutoka na kukusanya vifaa vya kutengeneza kalamu kwa wingi.
Uthubutu, na upambanaji wa Dkt. Mengi umemfanya hadi sasa kuwa mmoja wa matajiri wakubwa nchini na pengine ukanda wa Afrika Mashariki akiwa na biashara ya vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mfalme amuoa mlinzi wake na kumpa hadhi ya Malkia
Dkt. Mengi aliorodheshwa na jarida la Fobes mwaka 2014 kuwa na utajiri upatao Dola za Marekani 560 milioni, zaidi ya Sh za Kitanzania Trilioni 1.2 akiwa nafasi ya 45 kati ya matajiri 50 zaidi barani Afrika.
Hizi hapa ni moja ya heshima na tuzo alizo tunukiwa Dkt. Mengi katika uhai wake;
- 2000-2003 – Most Respected CEO East Africa Community (EAC)
- 2008 – Martin Luther King Drum Major for Justice Award
- 2010 – Global Leadership and Humanitarian Award
- 2012 – United Nations NGO Lifetime Achievement Award
- 2012 – The Business for Peace Award
- 2012 – Honorary Doctor of Humanity Degree Award
- 2014 – International Order of the Lions Award
- 2014 – Business Leader of the Year Award
Pumzika salama Dkt. Reginald Abraham Mengi. Amen