Halmashauri zote nchini zimetakiwa kukomesha ajira za watoto migodini na wadau wa Madini wakiongizwa na Wizara kukagua Migodi mara kuwa mara ili kudhibiti uharibifu wa mazingira.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ametoa tamko hilo leo Agosti 12, 2022 Jijini Dodoma katika maadhimisho ya miaka 50 ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO).
Dkt Mpango ameitaka wizara ya Madini kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kuhakikisha wanaboresha mazingira ya wachimbaji wa madini na kuboresha vitendea kazi ili visilete madhara kwa wachimbaji.
“Bado kuna migodi haizingatii utunzaji wa mazingira wanaachia maji machafu yenye madini ya Zebaki kuingia kwenye vyanzo vya maji hivyo kuleta madhara kwa wananchi. Niwatake wizara husika, STAMICO na NEMC kudhibiti jambo hili haraka kabla halijaleta matatizo makubwa,” amesema Dkt.Mpango.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko amelitaka shirika hilo kuhamishia nguvu katika biashara ya kiushindani kimataifa na kupongeza kwa mafanikio iliyoyaleta kwenye sekta ya Madini ambapo zaidi ya ajira 700 zimezalishwa ndani ya mgodi wa Kiwira.
Akizungumza Mafanikio ya Shirika hilo Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema shirika limefanikiwa kufufua mgodi wa Kiwira ambao ulikufa toka mwaka 2012, pamoja na kusaini mkataba wa kuuza makaa ya mawe elfu sitini yenye thamani ya shilingi bilioni nne.
Dkt. Mwasse amesema licha ya kuwepo kwa mafanikio makubwa katika shirika hilo lakini bado zipo changamoto zinazowakabili ikiwemo uhaba wa wafanyakazi, na taratibu za ununuzi wa umma bado sio rafiki kwa biashara.
Shirika la Madini la Taifa STAMICO limesherekea miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kwa kutoa gawio la shilingi bilioni 2.2 kwa serikali ikiwa ni sehemu ya faida yake.