Eva Godwin – Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amezitaka NGOs kuandika changamoto zote za kikodi na kuzipeleka Wizara ya Fedha, ili zifanyiwe kazi haraka na kusisitiza Watendaji wa Serikali wasiwe kimya wanapoandikiwa barua na badala yake wazijibu kwa wakati na kwa lengo husika.
Dkt. Mpango ameyasema hayo hii leo Oktoba 5, 2023 wakati akifungua jukwaaa la mwaka la NGOs Jijini Dodoma na kuongeza kuwa Watendaji hao wanapaswa kuimarisha ushirikiano na NGOs za nchi zingine, ili kujenga ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zao.
Amesema, “NGOs zote natoa wito kuimarisha ushirikiano na NGOs za nchi zingine ili kuweza kujenga ufanisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali, lakini pia NGOs zote mnapaswa kuzingatia na kutunza maadili ya Kitanzania katika utekelezaji wa miradi yenu, miongozo inayoratibu mashirika yenu izingatiwe.”
Kuhusu mabadiliko ya Tabianchi, Dkt Mpango amesema Serikali inaendelea na uhimizaji wa kupanda miti na uendelezaji wa shughuli za maendeleo katika kukabiliana na athari hizo na kuzipongeza NGOs zinazounga juhudi huku akitoa wito kwa mashirika yote, kuendelea kutoa elimu kwa wanachi kuhusu kutunza mazingira katika Maeneo yao.
Aidha, amesema ameridhia ombi la Mwenyekiti wa Bodi ya NaCoNGO kwa kuelekeza Mamlaka za Mikoa na Wilaya kufanya kazi kwa karibu na NGOs ili kuziwekea mazingira mazuri ya ufanyaji kazi huku Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima akisema wameendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwemo kuanzisha madawati ya uratibu wa NGOs katika sekta mbalimbali.