Kanisa la Wabaptist Tanzania limeiomba Serikali kupitia upya sheria za usajili wa Jumuiya za kidini hapa nchini.
Ombi hilo limetolewa na Viongozi wakuu wa kanisa hilo wakiongozwa na Askofu Mkuu Anorld Manase walipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Wamesema hatua ya kupitiwa upya kwa sheria za usajili wa Jumuiya za kidini, itasaidia kulinda misingi iliyowekwa kutokana na kuongezeka kwa huduma hizo hapa nchini.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa hilo Anorld Manase ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa uhuru wa kuabudu kwa makanisa yote hapa nchini, na kuahidi kuwa kanisa la Wabaptist Tanzania litaendelea kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango amewashukuru Viongozi hao pamoja na waumini wote wa kanisa hilo kwa kuendelea kuliombea Taifa, ili liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano.
Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, jamii yeyote yenye maadili mema na uzalendo inatokana na mchango mkubwa unaotolewa na Viongozi wa dini.
Amesema kanisa la Baptist limekuwa na mchango mkubwa katika kushirikiana na Serikali kutoa huduma za kijamii ikiwemo elimu na afya, hivyo amewaomba kuendelea kutoa huduma hizo ikiwemo kufungua upya Chuo Kikuu walichokuwa wanakimiliki hapo awali cha Mount Meru.
Amewahakikishia Viongozi wa dini nchini kuwa Serikali itaendelea kupokea ushauri na maoni kutoka katika taasisi za dini na kuahidi Serikali itazifanyia kazi changamoto zote zilizotolewa na kanisa la Wabaptist Tanzania