Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Mhimili wa Mahakama kushiriki kikamilifu katika kazi ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 pamoja na maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo 2050 ili kuenda sambamba na mfumo wa sheria na utawala bora unaohitajika utakaolingana na mikakati ya kiuchumi.
Makamu wa Rais ameyasema hayo hii leo Aprili 12, 2023 wakati akifungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na kufanya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 unaofanyika katika Ukumbi wa Malaika mkoani Mwanza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akihutubia Majaji pamoja na watumishi wa Mahakama wakati akifungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na kufanya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025.
Amesema, katika kipindi cha miaka 25 ijayo Tanzania inatarajiwa kutumia rasimali zake, fursa mbalimbali, teknolojia na ubia wa kimkakati katika kupiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo na kufikia uchumi wa kipato cha juu hivyo Mhimili wa Mahakama unapaswa kutoa kipaumbele kushiriki ipasavyo katika zoezi hilo muhimu kwa mustakabali wa Taifa.
Aidha, Makamu wa Rais pia ametoa rai kwa Mahakama kuzingatia ufanisi wa shughuli za utoaji haki nchini kwa kutambua kwamba ni nguzo muhimu ya kulinda amani na utulivu katika nchi lakini pia kukuza utawala wa sheria pamoja na shughuli za kiuchumi, biashara na uwekezaji.
Amewasisitiza Majaji, Mahakimu, na watumishi wote wa Mahakama kutumia Mkutano huo kujadili na kutathmini masuala muhimu yanayoathiri utendaji wao na kuandaa mapendekezo yenye tija ambayo yataongeza ufanisi na kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma ametoa wito kwa wananchi kufuata taratibu katika njia za utafutaji haki kisheria kabla ya kufikisha malalamiko kwa viongozi wa serikali. Amesema zipo njia sahihi ikiwemo kutoa taarifa kwa taasisi zinazosimamia maadili pale mwananchi anapoona hajatendewa haki na ukiukwaji wa maadili umefanyika.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma wakati alipowasili katika Ukumbi wa Malaika Jijini Mwanza kufungua Mkutano wa Majaji wa Tathimini ya Utendaji wa Mahakama na kufanya Mapitio ya Mpango Mkakati wa Mahakama 2020/2021 – 2024/2025 leo Aprili 12, 2023.
Amesema Mkutano huo ni nafasi kwa watumishi wa mahakama na wadau mbalimbali kwa kuwa tathimini inayofanyika inagusa sekta zote za uchumi, siasa pamoja na huduma. Aidha ameongeza kwamba mkutano huo ni fursa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa kuwa watapata nafasi ya kufahamu maboresho mbalimbali ili kuzingatia kwamba majalada wanayoamua yanahusu maisha ya watu na uchumi.