Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amezitaka Kampuni kubwa na za kati kuchangamkia fursa ya uwepo wa Sekta ya Soko la Mitaji, kwa kujiorodhesha katika soko la hisa la Dar es salaam ili kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa uchumi wa nchi.
Ameyasema hayo Bungeni Mjini Dodoma, wakati akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la Magomeni, Jamal Kassim Ali, aliyetaka kujua mchango wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es saam (DSE), kwa wafanyabiashara wazawa.
Amesema kuwa kampuni kadhaa, ikiwemo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), TOL Gases, Kiwanda cha Sigara (TCC), Kiwanda cha Saruji Tanga, Wakala wa Huduma za Mizigo kwenye viwanja vya ndege-Swissport na Benki ya NMB, ni baadhi ya kampuni zinazouza hisa zake katika Soko la Hisa la Dar es salaam.
“Kwa mfano kwa mwaka 2015 NMB, ilitoa gawiwo Serikalini kiasi cha shilingi bilioni 16.5 na TCC shilingi billion 1.4 kwa hisa zinazomilikiwa na Serikali huku mapato yatokanayo na kodi pamoja na gawiwo, hutumiwa katika kutoa huduma mbalimbali ambazo jamii ikijumuisha wafanyabiashara wadogo hunufaika nazo”amesema Dkt. Mpango
Hata hivyo, amebainisha kuwa Serikali inatambua mchango mkubwa wa kampuni ndogo ndogo katika kukuza uchumi wa nchi ndio maana mwaka 2013 Soko la Hisa la Dar es Salaam lilianzisha dirisha linaloziwezesha kampuni ndogo na za kati za wazawa zisizokidhi vigezo vya kujiunga na soko hilo kupitia dirisha kuu, kutumia Soko la Hisa katika kupata mitaji kutoka kwa umma wa watanzania.