Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amewasihi watanzania kutatua migogoro ndani ya familia kwa njia bora na sahihi zaidi ili kuepukana na athari zinazowakumba watoto ikiwemo kubaki yatima.
Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea kituo cha watoto yatima cha Jerusalem Home of God’s Love ForChildren kinachohudumiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kimara Jijini Dar es salaam.
Amesema ni muhimu kila mtanzania kuguswa na kutambua ni kosa mbele ya Mwenyezi Mungu na jamii kutupa mtoto ambaye ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ametoa wito wa familia kujiepusha na ugomvi na migorogoro na pale inapotokea basi yafaa kutumia njia bora za utatuzi kama vile dini, wazee na serikali.
Makamu wa Rais amezipongeza taasisi za dini nchini kwa kuendelea kujitoa kuhudumia watoto yatima na wale wanaopitia mazingira magumu. Aidha amewashukuru viongozi wa dini kwa kuendelea kuhubiri amani, kuombea viongozi wa nchi pamoja na kuliombea taifa.
Pia Makamu wa Rais ametoa shukrani za pekee kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani Usharika wa Kimara Jijini Dar es salaam kwa fikra za kuhakikisha kituo hicho cha watoto yatima kinakuwa endelevu kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika elimu na huduma za afya na kituo cha malezi kwa wazee.
Ameongeza kwamba suala la kuanzisha kituo cha huduma za afya pamoja na hospitali kwaajili ya kufundisha wataalamu wa afya katika eneo hilo litakuwa msaada kwa watoto yatima wanaolelewa hapo, jamii ya eneo hilo pamoja watanzania kwa ujumla.
Ametoa wito kwa watanzania kuacha tabia ya uvamizi katika maeneo ya taasisi za dini. Pia amesema ni muhimu kuhakikisha maeneo ya taasisi za dini yanapimwa mapema ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.
Dkt. Mpango amewahimiza waumini na watanzania kwa ujumla kuona ni wajibu kutunza nchi kwa kupanda miti na usafi wa mazingira kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.